BAVICHA YAILAUMU CCM

Posted by Bernard James on 1:30 AM with No comments

BARAZA la Vijana la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (BAVICHA), limelaani vikali njama walizodai kufanywa na Chama Cha Mapinduzi (CCM), kutengua kanuni ili waweze kuliteka Bunge Maalumu la Katiba kwa kupitisha maoni yao badala ya maoni ya wananchi yaliyowasilishwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.

Katibu wa BAVICHA, Bw. Deogratias Munishi, aliyasema hayo Dar es Salaam jana wakati akizungumza na waandishi wa habari na kusisitiza kuwa, kutengua kanuni hizo ni kuwakosea adabu wananchi wenye kiu ya kupata Katiba Mpya.
Alisema mfumo wa muundo wa Serikali uliopendekezwa katika Rasimu ya Pili (Serikali tatu), ndio inayofaa kudumisha umoja na mshikamano wa Watanzania tofauti na mfumo wa Serikali mbili unaopendekezwa na CCM.
 

Alisema Serikali ya CCM inaandika Katiba Mpya kwa shinikizo la wananchi hivyo lazima watambue kuwa, wananchi walioshinikiza ndio hao ambao watasimama kidete kupata katiba wanayoitaka ambapo vijana wote lazima watambue kuwa, chama tawala hakina mpango wa kuona nchi inapata Katiba Mpya.
 

"BAVICHA inalaani vikali njama zinazofanywa na CCM kutaka kuharamisha kanuni ili kuliteka Bunge hili, mfumo wa Serikali mbili unaopendekezwa na CCM umepandikiza chuki miongoni mwa wananchi waishio pande mbili za Muungano," alisema.
 

Bw. Munishi aliongeza kuwa, hotuba ya Rais Jakaya Kikwete aliyoitoa hivi karibuni katika Bunge hilo, imeleta mgawanyiko miongoni mwa wajumbe badala ya kuleta maridhiano kwenye mambo ambayo yatakuwa magumu kuamuliwa na wajumbe.
 

Aliwataka wananchi kukataa kuburuzwa au kushuhudia Katiba mbovu inapatikana na kuivumilia CCM pamoja na wapambe wake ambao wameamua kuhujumu maoni yaliyomo kwenye Rasimu ya Pili kupitia Bunge hilo.